logo

WADAU WA KISWAHILI WAHIMIZWA KUZINGATIA UMUHIMU WA LUGHA

Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi ikishirikiana na Idara ya Jinsia, Ulinzi wa Kijamii na Utamaduni katika Gatuzi la Uasin Gishu Ijumaa iliandaa warsha ya maafisa wa mawasiliano na wanahabari pamoja na wadau wa sekta ya kiswahili mjini Eldoret.

Warsha hiyo iliongozwa na Afisa mkuu wa Utamaduni Bi. Eunice Suter na ilipania kuendeleza uhamazisho wa kukuza lugha ya Kiswahili.

Akizungumza wakati wa halfla hiyo, Bi. Suter aliwahimiza washiriki na wadau wengine wa Kiswahili kuzingatia umuhimu wa lugha hii na kuitumia kwa wingi katika mawasiliano na maisha ya kila siku.

Aidha, alisisitiza kuwa Kiswahili ni sehemu muhimu ya utamaduni wa taifa, ikichangia uwuiano na maridhiano, kwa hivyo inapaswa kutunzwa na kutumiwa kwa heshima katika maeneo yote.

Wadau pia walichangia kuwa sera zinafaa kuwekwa ili kuona kuwa lugha ya Kiswahili inahimizwa kwa watoto walio katika viwango vya chekechea.

Mkurugenzi wa idara ya utamaduni katika Gatuzi la Uasin Gishu, Mohamed Haji, ambaye alikuwepo katika mafunzo hayo, alisisitiza kuwa lugha ya Kiswahili ni utamaduni kivyake.

Alitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa kuendeleza na kusambaza matumizi ya Kiswahili katika jamii.

Kwa pamoja, wadau hao walikubaliana kuendelea kushirikiana kukuza lugha ya Kiswahili na kuieneza zaidi ili iweze kustawi na kutambulika kimataifa.

Mafunzo hayo yalikuwa hatua nzuri na msingi ya kuhamasisha matumizi ya Kiswahili na kuzidi kuifanya lugha hiyo kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya utamaduni na mawasiliano nchini.

Hatua hii inaonyesha jitihada zilizofanywa na serikali kukuza na kulinda lugha yao ya asili.